Jeshi la Polisi mkoani Rukwa nchini Tanzania linamshikilia kijana mmoja mkazi wa
Kijiji cha Mtenga Tarafa Namanyere wilayani Nkasi, kwa tuhuma za kumuua
babake kwa kumkatakata mapanga kichwani akidai urithi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo amesema kuwa tukio la
kuuawa kwa mzee huyo lilitokea wiki hii, majira ya saa 09:30 usiku huko Kijiji
Mtenga wilayani Nkasi.
Amesema, kijana huyo mwenye umri wa miaka 36 jina linahifadhiwa inadaiwa
alikuwa akitaka baba yake mzazi ampe urithi wa mali alizonazo ili ziweze
kumsaidia kupata kuendesha maisha yake pasipo utegemezi.
Masejo amesema, baada ya kijana huyo kushinikiza mara kadhaa apewe sehemu
ya mali ya mzazi wake kama urithi na baba yake kukataa kufanya hivyo kulizuka
vurugu baina yao ndipo kijana huyo alipochukua panga na kuanza kumkimbiza na
kisha kumkamata na kuanza kumkatakata kwa mapanga kichwani.
Vilevile Kamanda huyo amesema, Baba huyo alivuja damu nyingi katika sehemu
ya kichwa na kufariki dunia muda mfupi baadae kutokana na kukosa msaada wa
haraka wa ufikishwa hospitalini kwa matibabu.
Na kwa sasa mshukiwa huyo anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani
mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika.