Mastin Mukanga alifunga pingu za maisha na Linet Kavere mnamo Disemba 11,2020, katika harusi iliyofanyika katika bustani la Sosa nchini Kenya.
Wawili hao walikutana katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro wakiwa wanafunzi na kuanza kuwa marafiki wa dhati na kisha baadaye kuchumbiana baada ya kumaliza chuo.
Mastin alipata ajira kama Mhandisi katika Shule ya Msingi ya Phanero mjini Mbale huku Linet akipata nafasi ya kufunza Kizungu katika Shule ya Wasichana ya Mbihi.
Wakati wanandoa hao walirejea kutoka kwa fungate yao, walikuwa wanaazimia kuishi maisha ya raha mstarahe hadi kifo kitakapowatenganisha.
Lakini walitenganishwa siku 18 baada ya siku yao ya harusi.Siku moja tu baada ya fungate Linet alianza kukumbana na matatizo ya kupumua, akazirai na kisha kukimbizwa katika Hospitali ya Kisumu Specialists ambapo alithibitishwa kufariki saa chache baadaye.
Humphrey Odanga, mwalimu mkuu wa Mbihi, ambapo marehemu alikuwa akihudumu, alimsifu Linet kwa kuwa mwalimu mwenye bidii.
โAlikuwa nasi karibia miaka miwili na kando na kuugua magonjwa ya kawaida kama mtu yeyote yule, hakuonyesha dalili zozote za kuwa na changamoto za kiafya,” alisema.
Linet alizikwa Jumamosi, Januari 9, 2021, saa tatu baada ya mwili wake kuwasili kutoka makafani kulingana na sheria za COVID-19 nchini Kenya.
Matokeo ya upasuaji yalionyesha kuwa Linet alikumbana na shinikizo la damu kwenye mishipa kitu ambacho kilisababisha kifo chake.