Mamilioni ya miaka iliyopita, waliishi wanyama hawa. Wanyama hawa walikuwa ni wakubwa na walikuwa ni katika jamii ya mijusi (reptiles).
Dinosaur waliishi duniani na kuwa ndio wanyama wa pekee wenye nguvu kwa zaidi ya miaka milioni 165. Kipindi hicho mabara yalikuwa bado hayajajigawanya na kuwa mabara tofauti kama tuliyonayo hivi sasa, waliishi katika bara moja tu lijulikanalo kama Pangaea. Lakini sasa wanyama hawa hawapo tena duniani kwa muda wa miaka milioni 65 sasa. Wanapaleontolojia waligundua mabaki yao katika sehemu ambayo kwa sasa inajulikana kama Argentina na kuyachunguza na kuyajadili kwa undani zaidi kujua habari ya wanyama hao.
Dinosaur waliishi nchi kavu na kutembea wima kama wanyama wengine. Nyonga zao za kipekee zilifanya miguu yao inyooke na kuweza kubeba miili yao na bila ya kutambaa kama aina nyingine ya mijusi kama vile kenge, mijusi yenyewe na mamba.
Mwanzoni kabisa wanyama hawa waliweza kutembea kwa miguu miwili, lakini baadaye baadhi ya kundi la wanyama hawa walianza kutembea kwa miguu minne kama walivyo wanyama wengine wakiwa na miguu ya nyuma mirefu sana kuliko miguu ya mbele.
Kulikuwa na aina mbalimbali za dinosaur, wengine walikuwa wakubwa sana, wengine walikuwa wadogo, kuna wengine walitembea kwa miguu minne, na wengine walitembea kwa miguu miwili, kuna wale walikuwa na mbio sana, wengine walikuwa wakitembea taratibu sana, wengine walikuwa wala nyama (carnivores), wengine walikuwa wala majani (herbivores),wengine walikuwa na mapembe, wengine walikuwa na ngozi ngumu.
Dinosaur walikuwa duniani kabla ya kuja kwa binadamu.Kwa hivyo Mpaka sasa hakuna anayefahamu kwamba wanyama hawa walikuwa na rangi gani kwani hajaonekana hata mmoja akiwa hai bali ni mifupa yao tu ndiyo iliyoonekana. Na pia hakuna ajuaye kuwa walikuwa na sauti ya aina gani, au walikuwa na tabia zipi, au hata mabaki hayo hayakuweza kutambulika kama ni ya kike au kiume.
Dinosaurs kwa sasa hawapo tena kwa muda wa miaka milioni 65 iliyopita, na sababu kubwa inasemekana ni kutokana na kwamba kipindi hicho kulikuwa na milipuko ya volcano pamoja mabadiliko makubwa sana katika ardhi. Lakini theory ambayo imekubalika na wataalamu wengi ni kwamba asteroid iliyodondoka wakati huo ilisababisha badiliko kubwa sana la tabia ya nchi (climate change) ambayo ilikuwa haiwaruhusu wao kuishi katika hali hiyo na hatimaye kufa wote kabisa.
Lakini pia kuna wataalamu wengine wanasema kuwa kuna aina ya ndege ambao wanahesabiwa kuwa dinosaur ila uhakika kamili haupo na wapo hai mpaka sasa.