Watoto wa shule nchini Kenya huenda watasalia nyumbani mwaka huu wote iwapo haitapatikana chanjo au tiba ya homa kali ya Corona ambayo imesambaratisha kila kitu kote duniani.
Ni kauli ya hivi punde ya waziri wa elimu nchini Kenya,Profesa George Magoha,ambayo ameitoa akiwa mbele ya kamati ya bunge ya kitaifa na kusema kuwa hadi sasa haijulikani ni lini shule zitafunguliwa. Na la muhimu kwa sasa ni serikali kuhakikisha afya ya wanafunzi na kuwarai wabunge kutenga pesa za kutosha kwa shule kununua barakoa,dawa na hata madawati zaidi shule zitakofunguliwa.
Ikumbukwe kwamba kwa sasa wanafunzi wote nchini Kenya wanapata mafunzo kupitia kwa mitandao,redio na runinga.Na wanatakiwa kuendelea kupokea mafunzo hayo hadi pale shule zitakapofunguliwa.