Wiki chache tu baada ya Mwanasiasa mkongwe Simeon Nyachae kufariki dunia, eneo la Gusii limerejea tena kwenye maombolezi kufuatia kifo cha Mbunge wa Bonchari Mhe. John Oroo Oyioka aliyefariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan wakati akipokea matibabu.
Afya ya Mhe. John Oroo ilianza kuangaziwa baada ya mwanasiasa huyo kuanguka huko Kisii mwishoni mwa mwaka jana, na kukimbizwa hospitalini ambapo alilazwa hadi kifo chake leo.
Amekuwa mbunge wa eneo bunge la Bonchari kutoka 2017 kupitia tikiti ya Chama cha People’s Democratic (PDP).
Mbunge huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa muda mrefu ambapo familia haijaweka wazi kilichokuwa kikimsumbua wakati huo wote, na kusababisha aanguke akiwa kazini. John Oroo ni mwanasiasa na kiongozi wa pili kufariki dunia eneo hilo la Kisii mwezi huu wiki moja baada ya mkongwe Simeon Nyachae kuaga dunia.