Mchungaji wa kanisa la Akorino katika kijiji cha Kianyakiru eneo bunge la Ndia, Kaunti ya Kirinyaga ambaye alikiri kuwanajisi na kuwapachika mimba binti zake wawili anatarajiwa kuhukumiwa wiki ijayo nchini Kenya.
Mchungaji huyo mwenye umri wa miaka 51 alikiri kosa hilo na kumlaumu shetani kwa kumsukuma kutenda uhayawani huo na pia akaomba Mahakama inayoshughulikia kesi za watoto imsamehe.
Hakimu mwandamizi Anthony Mwicigi alisema mchungahi huyo alikiri kosa lake na akaamuru hukumu dhidi yake kufanywa Januari 14, 2021.
Kulingana na mashtaka, mshukiwa anaaminika kuwatendea unyama huo mabinti zake wenye umri wa miaka 14 na 16 kws mara ya kwanza kati ya tarehe mosi na 30 mwezi Juni, 2019 na kwa mara ya pili kati ya tarehe mosi na 31 Agosti 2020.
Mwendesha mashtaka mkuu Patricia Gikunju aliiomba korti kuipa timu yake hadi Januari 7 kukusanya vyeti vya kuzaliwa kwa watoto hao na stakabadhi zingine zinazothibitisha umri wao.Na hivyo mshukiwa ameshikiliwa katika kituo cha polisi cha Sagana.
Mchungaji huyo alikamatwa Jumapili eneo bunge la Mbeere Kusini akiwa mafichoni baada ya maafisa wa polisi kuanza msako dhidi yake mwezi jana.