Miongoni mwa majina ya wagombea ubunge yaliyopitishwa Agosti 20, 2020 na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni la Hamis Taletale maarufu kama BABU TALE, ambaye sasa ndiye mgombea wa ubunge Jimbo la Morogoro Mashariki mkoani Morogoro.
Licha ya kupitishwa na kamati kuu, Babu Tale pia ambaye ni Meneja wa Msanii wa Bongofleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platinumz’, alishinda kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.
Mwingine kutoka tasnia ya burudani aliyepitishwa na CCM Kugombea ubunge ni msanii wa muziki wa kizazi kipya ya kufoka foka (HipHop), Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA ambaye aliyepitishwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kukiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu kwenye nafasi ya Ubunge jimbo Muheza mkoani Tanga.Licha ya Mwana FA kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye mchakato wa kura za maoni,chama cha Mapinduzi kiliamua kumchagua na kuwaacha wagombea wenza.
Kupitishwa kwa wagombea hao kutoka tasnia ya Burudani na Muziki wa kizazi kipya nchini ni ongezeko la wasanii mbalimbali kutaka kuongeza nguvu bungeni, baada ya uwepo wa wasanii kama Joseph Haule ‘Profesa Jay’ mbunge wa Mikumi, Vicky Kamata,.Joseph Mbilinyi maarufu kama SUGU ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini na Khadija Shaban ‘Keisha.’