Mtoto mvulana wa umri wa miaka 6 amefariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa kung’atwa na fisi katika eneo la Relini – Nhelegani Mjini Shinyanga nchini Tanzania.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba tukio hilo limetokea Agosti 1,2020 majira ya saa 12 jioni wakati mtoto huyo akiwa njiani kurudi nyumbani akitokea kuchunga ng’ombe akiwa na watoto wenzake.
Mvulana huyo aitwaye Kulwa Machiya alijeruhiwa kwa kung’atwa na fisi sehemu za usoni na kusababishiwa majeraha makubwa usoni wakati akiwa njiani kurudi nyumbani akitokea kuchunga ng’ombe akiwa pamoja na watoto wenzake kisha fisi huyo kuingia vichakani baada ya kusikia mayowe ya watoto hao waliokuwa na kulwa.
Kamanda Magiligimba amesema elimu ya kujikinga na wanyama wakali imetolewa na anatoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuchukua tahadhari kwenye maeneo yao kwani kipindi hiki yameripotiwa matukio mengi ya kuwajeruhi na kuwaua watoto walio na umri chini ya miaka 10 mkoani humo.