Polisi mkoani Maranchini Tanzania wanamshikilia mwanafunzi wa kidato cha tatu Mwita Machamo mwenye umri wa miaka 17, katika shule ya sekondari ya Kiagata kwa kumkata na panga mwalimu wake Majogoro John, baada ya mwanafunzi huyo kushindwa kumpeleka mzazi wake shuleni kama alivyoagizwa na mwalimu huyo.
Majogoro John ni mwalimu aliyejeruhiwa na mwanafunzi wake ameeleza kwamba alipita darasani majira ya asubuhi leo Septemba 24,2020 kuangalia watoro,akamuagiza mwanafunzi huyo afuate mzazi ili wajue shida ni nini hivyo mwanafunzi akamgeukia na kumkata na panga begani na alipotaka kumkata tena kichwani ndipo akaweka mkono wa kushoto na hivyo akakatwa mkono mpaka kuning’inia.
Mwalimu alipelekwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara na daktari wake Joachim Iyembe, amesema kuwa wamempokea mgonjwa huyo na kumpa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Baadhi ya wanafunzi waliwaleta wazazi wao, lakini huyu mwanafunzi kwa utovu wa nidhamu uliopindukia alikuja na upanga akiwa ameuficha kwenye nguo zake na mwalimu alipohoji kwanini hujaja na mzazi, mwanafunzi akachomoa upanga na kumshambulia mwalimu na akawatisha tisha wanafunzi wengine akapata nafasi ya kukimbia lakini wakamkata na tumemshikilia na atafikishwa mahakamani”, amesema Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Daniel Shillah.