Mwanamuziki Amelia Nambala kutoka Uganda ametiwa mbaroni na anashikiliwa na polisi baada ya kupatikana na vyeti 48 vya kusafiri.
Kwa mujibu wa taarifa za Daily Monitor, mwanamuziki huyo alikuwa ameandamana na rafikiye wakati walinzi wa Hoteli ya Sheraton waliposhuku kwamba alikuwa amebeba vifaa visivyo hitajika kwenye begi lake. Walinzi waliwaarifu maafisa wa polisi ambao walimkamata Nambala akiwa kwenye chumba kimoja cha kulala na mwenzake hotelini humo. Baada ya kupekua na kukagua begi laki, polisi waliweza kupata vyeti vya watu 48 vya kusafiri.
Hata hivyo,akijitetea, mwanamuziki huyo alisema kwamba alikuwa anapanga safari ya kuwapeleka watu hao nchini Uturuki lakini hakuelezea ni kwa ajili ya sababu ipi. Nambala na mwenzake aliyetambulika kama Esther Nassali wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kampala Central huku uchunguzi dhidi yao ukiendelea.
Amelia Nambala anashukiwa kushiriki katika biashara ya ulanguzi wa binadamu lakini maafisa wa polisi wamesema bado wanafanya uchunguzi dhidi yake.
Inasemekana sio mara ya kwanza kwa msanii huyo kupatikana katika mkono mbaya wa sheria kwani amewahi kukamatwa tena kwa kuhusika katika ufisadi mwaka wa 2019. Nambala alikashfiwa kwa kumtapeli jamaa mmoja aliyetambulika kama Sekandi KSh 210, 000 ili amtafutie visa ya kuwawezesha watoto wake kusafiri kwenda Sweden ahadi ambayo hakutimiza.