Mwanaume wa miaka 70 na mtoto wake mvulana wa miaka 28 wamefikishwa mahakamani Machakos leo kwa kushtumiwa kumnajisi msichana wa miaka 11 ambaye ni mjukuu wa mwanamme huyo wa miaka 70 na mpwa wa mvulana huyo wa miaka 28 katika kijiji cha Kathiani nchini Kenya kwa miaka minne.
Mahakama iliomba wawili hao ambao ni James Muia (babu wa msichana ) na Benjamin Mutinda Muia (mjomba wa msichana huyo) wawekwe korokoroni kwa siku 5 hadi 7 ili kuwawezesha polisi kukamilisha uchunguzi wao kwa ajili ya kuwashtaki.Na kwa kuhofia kwamba wakiachiliwa kwa dhamana huenda wakaharibu uchunguzi kwa kuwa ni wanafamilia wa msichana huyo.
Wawili hao watarudishwa mahakamani tarehe 4 na 6 mwezi wa nane mwaka huu.
Kwa kosa hili iwapo mtu amepatikana na hatia ya kumnajisi mtoto asiyezidi miaka 11 au wa miaka 11 anastahili kufungwa kifungo cha maisha.
Wakati huohuo mama ya msichana huyo pamoja na wanawe wamefukuzwa kutoka nyumbani kwa mumewe kwa madai kwamba ameaibisha familia yao kwa kuripoti kisa hiki kwa polisi.Kwani walitaka wayamalize kinyumbani.
“Baada ya washukiwa wa kitendo hicho kutiwa mbaroni, mzee wangu ameniumiza moyo, ameniambia mimi ni muuaji na sifai kuwa hapa, nibebe watoto wangu wote niende, watu wa familia walifanya mkutano na hawakutaka kunihusisha nijue wasema nini,” amesema mama ya msichana huyo.
Mama ya msichana huyo kwa sasa hayupo nyumbani na ameiomba serikali kumhakikishia usalama wake na wanawe na kuhakikisha haki inatendeke kwa mwanawe.