Rais wa Rwanda Paul Kagame ametangaza maombolezo ya Kitaifa Rwanda kufuatia kifo cha Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na ameagiza Bendera ya Rwanda na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zote zipeperushwe nusu mlingoti nchini humo kuanzia leo June 13 hadi siku Nkurunziza atakapozikwa.
Wakati huo huo, Katiba ya Burundi inaeleza kuwa spika wa bunge anatakiwa kuchukua nafasi ya rais wa mpito pale rais anapofariki lakini mahakama ya kikatiba ya nchi hiyo imeamua kuwa, kwa kuwa tayari kuna rais mteule ambaye bado hajaapishwa hivyo rais mteule huyo, Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye aapishwe urais mara moja
ili kuchukuwa hatamu ya uongozi wa nchi.
Hukumu hii ya Mahakama ya Katiba inamaliza sintofahamu iliyokuepo kuhusu nani atakaye chukua nafasi ya rais baada ya rais Pierre Nkurunziza kufariki dunia ghafla Jumatatu Juni 8 kutokana na “shinikizo la moyo” kwa mujibu wa serikali ya Burundi.
Ndayishimiye wa chama tawala cha CNDD-FDD aliyechaguliwa Mei 20 awali alikuwa aapishwe mwezi Agosti mwaka huu wa 2020.