Msanii wa muziki kutokea nchini Nigeria, Lil Frosh amezuiliwa rumande katika gereza la Ikoyi mjini Lagos kwa madai ya kumshambulia mpenzi wake maarufu kama Gift Camille.
Lil Frosh mwenye umri wa miaka 22, alikana shtaka hilo mbele ya Hakimu Adeola Olatunbosun, Jumanne, Februari 9, 2021, ambapo kesi hiyo iliahirisha hadi Machi 9, 2021.
Itakumbukwa Oktoba 2020, Lil Frosh alikumbwa na tuhuma za kumtembezea kichapo na kumuumiza vibaya binti huyo mwigizaji na mwanamitindo mwenye umri wa miaka 21.
Madai hayo dhidi ya Lil Frosh yalitolewa sambamba na picha kadhaa zilizosambazwa mtandaoni zikimuonesha binti Camille akiwa amejeruhiwa vibaya usoni.
Mara baada ya madai hayo dhidi ya Lil Frosh, lebo ya msanii Davido, Davido Music Worldwide ‘DMW’ iliyokuwa imemsaini, katika kupiga vita unyanyasaji wa aina hiyo, ilisitisha mkataba na msanii huyo.