Serikali ya Kenya imesema kwamba kufikia sasa fedha zilizotumika ni shilingi bilioni themanini na nne.Huku wakenya wakiwa na maswali mengi kuhusu namna kiwango hicho cha fedha kilivotumikakatika mipango yote ya kukabili janga la korona nchini humo.
Waziri wa Fedha Ukur Yattani amesema fedha hizo ni sehemu ya shilingi bilioni mia moja thelathini na nne ambazo serikali ya Kenya imepokea kutoka kwa mashirika mbalimbali yakiwamo yale ya kimataifa. Yattani amesema Wizara ya Fedha ndoyo imepokea kiwango cha juu cha fedha ambazo ni shilingi bilioni 10.2.
Akizungumza alipohojiwa na Kamati ya Bunge ya Afya, Waziri Yattani aidha amesema Serikali za Kaunti zimepokea shilingi bilioni tano, ambazo zitatumika katika kukabili janga la Korona kukiwamo kuwalipa marupurupu wahudumu wa afya.
Aidha amewaeleza Wabunge kwamba fedha nyingine bilioni 1.5 zimetengewa baadhi ya Hospitali ambazo zinawahudumua wagonjwa wengi wa COVID-19 na nyingine milioni mia nane hamsini zikitengewa makundi ya watu wasiojiweza kwenye Kaunti nne.
Pia amesema mipango ya ufufuaji uchumi ambao umedhorora kutokana na korona inaendelea na kiasi fulani cha fedha kitatengwa kuifanikisha.
Ikumbukwe kumekuwapo na madai ya ufisadi hasa kuhusu ununuzi wa vifaa vya kujikinga PPEs , madai ambayo Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ameyapuuza akisema bei ya bidhaa hizo ilitokana na hitaji kote duniani wakati ambapo mataifa mengi yalikuwa yameanza kurekodi visa vingi vya maambukizi.
Sasa Waziri Kagwe ameagizwa kufika mbele ya Kamati hiyo Jumatatu kuhojiwa, baada ya wabunge kukataa kumpa nafasi Katibu wa Wizara ya Afya Susan Mochache aliyekuwa ametumwa kumwakilisha Kagwe katika kikao cha juzi.