Leo ikiwa ni tarehe 7 mwezi wa saba yaani SabaSaba kumekuwa na maandamano jijini Nairobi nchini Kenya .Waandamanaji kutoka mitaa ya Kayole na Mathare leo walikumbana na vitoa machozi walipoandamana kuelekea katikati ya jiji la Nairobi katika kuadhimisha maandamano ya 30 ya siku ya sabasaba.Makundi kadhaa ya kijamii pamoja na wanachama mashuhuri wa vuguvugu la Sabasaba na wanaharakati walikuwa wamepanga maandamano kwa jina ‘Saba Saba Match for our lives’ kwenye barabara ya Harambee –Nairobi.
Hata hivyo polisi walikabili kundi hilo kabla yakuingia jijini na kuwatawanya kwa kutumia vitoa machozi.
Jinsi ilivyotangazwa na mwanaharakati Bonface Mwangi miongoni mwa wengine , maandamo hayo yalilenga kushinikiza utekelezaji kikamilifu wa katiba ilivyoratibishwa mwaka 2010.
Kundi hilo lilisema mafanikio ya vuguvugu la sabasaba yatapotezwa iwapo katiba hiyo haitatekelezwa kikamilifu.Ni miaka 30 tangu kuandaliwa maandamano ya kwanza ya sabasaba ambayo yalianzisha mchakato wa kubadilisha katiba na kuiwezesha Kenya kuwa na demokrasia ya vyama vingi.