Familia nzima ya watu 5,baba,mama na watoto wao watatu yapatikana imefariki dunia eneo la Githurai katika kaunti ya Kiambu nchini Kenya.
Familia hiyo inashukiwa kuvuta hewa yenye sumu ya carbon monoxide kutoka kwa jiko la kupikia la makaa lilikokuwa limewashwa. Akithibitisha kisa hicho Kamanda wa Polisi wa Ruiru, Phineas Lingera amesema mwanaume alikuwa muuza mahindi katika eneo la Githurai 45 na inashukiwa huenda alikuwa anapika chakula hicho kwenye jiko usiku. โTunaamini alilala sana na kusahau kuzima moto. Familia hiyo huenda ilifariki kutokana na kukosa hewa baada ya kuvuta carbon monoxide,โ alisema Lingera.
Aidha Lingera ameshikilia kuwa kwa sasa hakuna chanzo kingine cha vifo hivyo kwani miili yao haikuwa na majeraha.
Kama kawaida mwanaume huyo aliwahi kufungua biashara yake kila siku ,ila jana alichelewa kuamka ndiposa majirani walianza kuwa na wasiwasi. Walibisha kwake ambapo mlango wake ulikuwa umefungwa kwa ndani lakini hawakufunguliwa ndipo wakaingiwa na wasiwasi na kuwaita maafisa wa polisi.
Miili imepelekwa katika Hifadhi maiti ya Nairobi City.
Kisa hiki kimetokea siku moja tu baada ya Watoto wengine watano kufariki dunia katika eneo hilo la Githurai baada ya kuanguka katika eneo moja lililotelekezwa baada ya kusitishwa kwa ujenzi.
Watoto hao wenye umri wa kati ya miaka mitatu na saba walikuwa wakicheza katika eneo hilo ambapo sehemu moja ilipoporomoka na kuwafukia hali iliyosababisha vifo vyao.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Ruiru, Phineas Lingera alisema watoto hao walizama ndani ya maji yaliyokusanyika katika eneo hilo.